Njaa ya Bara la Afrika ni ya kujitakia?

February 16, 2006

BBC iliendesha mdahalo mzuri sana kati ya Nicholas Crawford toka WFP na Tajudeen Abdul-Rahem Wa Justice Afrika kuhusu chakula barani Afrika. Jamaa wa Justice Afrika anadai kwamba hakuna haja ya Afrika kupewa msaada wa chakula na anajaribu kuelezea kiini cha tatizo la njaa barani Afrika na jinsi misaada inavyolemaza bara hili. Mzungu wa WFP anatetea umuhimu wa msaada wa chakula. Kwa kweli nakusihi usome mdahalo huo hapa. Ni mdahalo poa mno

Advertisements

Kuua mwenzako Ni upendo?

February 16, 2006

Nchi ya Botswana imekumbwa na ongezeko la mauaji yanayotokana na wanaume kuwaua wapenzi wao. Mwaka 2005 peke yake inasemekana kulitokea vifo sabini. Wenyewe siku hizi wanaita “Passion Killings”. Botswana ni nchi ndogo- si kwa ukubwa wa eneo bali kwa idadi ya watu. Ina watu wapatao milioni moja na laki sita tuu. Halafu maambukizi ya Ukimwi ni ya kutisha. Takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 40 ya watu wazima walioambukizwa. hapohapo kuna ongezeko kubwa la vifo kutokana na ajali nyingi shauri ya uendeshaji mbovu hasa kutokana na kunywa pombe kupindukia. Sasa haya mauaji ya kina dada tena inaongezea idadi ya vyanzo vikuu vya vifo yaani UKIMWI na Ajali. Ni hatari. Wanaume hawa mara nyingi wakishaua nao hujiua kwa vile wanajua watakuja kuhukumiwa adhabu ya kifo. Soma habari hiyo hapa

Ongezeko la makusanyo ya kodi

February 15, 2006

Nilipokuwa napitia kwenye kibaraza cha Msaki Nimekuta mahali alipoongelea ziara ya Rais JK huko TRA. Kati ya mambo ambayo serikali ya Mkapa imeondoka madarakani ikijisifu kwamba imefanya vizuri ni ongezeko la makusanyo ya kodi. Walikuwa wakisema kwamba makusanyo yaliongezeka toka shilingi bilioni 25 kwa mwezi mwaka 1995 na kufikia bilioni 120 wakati fulani mwaka 2005. Ambacho hatukuambiwa ni ongezeko halisi. Kiuchumi ingeleta maana kama tungeambiwa hizo bilioni 125 za mwaka 2005 (miaka kumi baadaye) zina thamani gani. Kwa kweli njia rahisi ya kulinganisha mambo kama haya huwa ni shilingi bilioni 25 za mwaka 1995 zingeweza kufanya nini mwaka 2005. Kama hili halikuelezwa basi inaweza ikawa ni hadithi tuu. Pengine ukipiga mahesabu zingekuwa na thamani sawa. Jambo la pili ambalo tungefaa tuelezwe ni chanzo cha kodi hizi. Nadhani ukifuatilia utakuta mchango mkubwa unatokana na kodi ya mapato. Na kwa vile mwajiri mkuu ni Serikali basi inajilipa kodi yenyewe. Kwa jinsi ambavyo kumekuwa na tambo za ongezeko la wawekezaji basi tungetarajia kwamba “Cooporate Tax” ndiyo ingetoa mchango mkubwa katika kodi. Hilo bado halijawezekana. Kwa hivyo Changamoto iliyo nayo Serikali ya awamu ya nne ni kuziba mianya inayotumiwa na hao wawekezaji uchwara ili kuongeza “Cooporate Tax”. Vinginevyo kama hadithi hii ya ongezeko la kodi kutokana na kodi ya mapato itaendelea hatutafika mbali sana. 

Maisha yetu baada ya Miaka 50

February 15, 2006
Kwa wale wasomaji wa makala za Padre Karugendo, naweka makala yake moja ambayo aliiandika kama changamoto kwa waliofikisha umri wa miaka 50 mwaka huu. Yeye ni mmojawapo wa hao waliofikisha umri huo. Unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa

NEPAD ubeberu mpya

February 15, 2006
Kuna mjadala sasa kwamba hili dude linaloitwa NEPAD ni aina mpya ya ubeberu ambapo Afrika ya Kusini inatumia kupeleka mitaji katika nchi nyingine za Afrika. Kuna bwana mmoja kaandika kitabu juu ya hili. Lakini hata kusingekuwa na hicho kitabu hili ni jambo la wazi kabisa. Ukiangalia changamoto wanazokabiliana nazo hawa jamaa wa Afrika ya kusini utagundua kwamba ni ukweli mtupu. Baada ya ule mfumo wa kibaguzi kwisha mwaka 1994 ilibidi watafute nafasi ya kuwakuza kiuchumi weusi. Njia rahisi ilikuwa ni kuwatafutia weupe nchi za kupeleka mitaji yao ili nafasi ibaki nchini mwao kuwasaidia weusi. Nchi nyingi za kiafrika zimeingia kwenye makubaliaono hayo bila kuona janja ya hawa jamaa. Tatizo ni kwamba biashara inakuwa ya upande mmoja. Nchi nyingi sana hazina mtaji wa kuwekeza Afrika ya kusini. Kwa hivyo tutawasidia kupunguza matatizo yao huku hizo sera zikiwa hazisaidii sana nchi zingine. Wanapotoka kwenda nje hawana mpango wowote wa kuendeleza nchi wanazowekeza. lao ni kupata faida na kuondoka. Ubeberu huu mpya sijuhi utatufikisha wapi.

Gregory yuko wapi?

February 15, 2006
Nilikutana na binti mmoja ambaye tulikuwa wote Jeshi la Kujenga Taifa (Ndesanjo huliita la kubomoa taifa) akaniuliza: Hivi Gregory yuko wapi siku hizi? Nikamuuliza Gregory gani? Akanishangaa akasema kumbe urafiki wenu uliishia jeshini? Nikamuuliza jina lake la pili ni nani? Akaniambia Macha. Ohh!! Nikamwambia nimemkumbuka sasa. Nikamwambia kwamba Macha alirudisha jina lake la Gregory kwa Mchungaji wake kama mmoja wa wahusika katika kitabu cha Pambazuko Gizani alivyotaka kurudisha jina lake la Paulo kwa Padre. Binti wa watu hoi. Nakumbuka Macha alipokuwa kwenye jitihada za kurudisha jina lake alikuwa akinishambulia kila siku nirudishe la kwangu pia ikiwa ni ishara ya ukombozi mpya. Kabla ya kurudisha jina lake Ndesanjo alikuwa akiitwa Gregory!!!

Ilikuwa lazima Yesu afe?

February 15, 2006
Rafiki yangu mmoja ameniacha hoi aliponiuliza kwamba; hivi Mungu alikosa njia nyingine ya kumkomboa mwanadamu mpaka amtume Mwanae wa pekee afe kwa ajili ya dhambi zetu? Kulikuwa na ulazima wa damu kumwagika? Huyu jamaa yangu yeye si mfuasi wa dini za kuja kwa hivyo nikaona kwamba pengine anauliza mambo hayo kwa ajili hiyo. Baadaye nikaingia kwenye mjadala mwingine na jamaa mmoja mfuasi mzuri wa madhehebu ya kikristo. katika maongezi yake akasema angekuwa rais wa dunia angewaua watu wa jinsia moja wanaotaka kuooana. Jamaa akambana hivi wakristo mnaua? Nikapata jibu langu la awali la kwa nini Yesu afe? Jamaa alisema ndio maana Mungu alimtuma Yesu aje afe kutoa ishara kwamba hakuna ukombozi pasipo kumwaga damu!!

Mambo mengine! sijuhi tuanzie wapi

February 1, 2006
Mimi huwa ni kipofu wa dini. Inakuwa ngumu sana kwangu kumuuliza mtu dini yake au hata kuhisi kutokana na jina kwa sababu nimesoma na watu wenye majina ya kizungu ambayowengi huita ya kikristo lakini baadaye nikaambiwa ni waislamu wengine wenye majina ya kiarabu ambayo huitwa ya kiislamu baadaye naambiwa ni wakristo. Sasa huwa sichukulii jina kama kigezo kabisa. Sasa baada ya mawaziri kutajwa hapo Januari wengi wetu tulianza kujadili sifa zao. Lakini kuna jamaa wengine wameniacha hoi sana. Wanasema; wewe huoni Wizara nyeti zote kawapa waislamu? Angalia Fedha, Mambo ya nje akataja na Wizara nyingine lakini sikutilia maanani. Nikamuliza? Hivi Wizara kuwa nyeti maana yake ni nini? Au kwa mfano Kikwete alipokuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje kwa miaka kumi ambayo ni moja ya wizara nyeti kutokana na hao wanaodai hivyo waislamu walifaidi nini? Nilishangaa nikagundua kwamba kuna safari ndefu. Baadhi ya takwimu zinaonyesha kwamba Tanzania ina asilimia 35 ya ambao si waislamu wala wakristo. Hawa watapewa wizara ipi? Na hizo takwimu za wakristo na waislamu pwngine zinafuata majina na nyingine ni za zamani. Kwa mfano kuna maelfu ya watanzani wenye majina ya kikrito na kiislamu(kama yapo) ambao hawako kwenye hizo dini au walishajiondokea na kujichukulia ustaarabu wao. Tukiendelea na huu uhayawani tutafika mahali kila dhehebu litake kuwa na waziri. Na kuna madhehebu karibu 400 ya kikristo tuu Tanzania. Sijuhi itakuwaje. Lakini hao ambao hawako kwenye hizi dini mbili nani atawawakilisha? Ndesanjo kaongelea kiapo kwa kutumia vitabu; kitukufu na kitakatifu. Suala linarudi niliyowahi kusema huko nyuma: elimu ya dini

Tumepoteza maelfu ya miaka ya elimu

January 19, 2006
Hivi lile Sakata la kufukuzwa kwa madaktari limeishia wapi? Kama wote walifukuzwa basi ni kwamba taifa limepata hasara ya maelfu ya miaka iliyowekezwa kwenye elimu. Tunaambiwa kwamba, kila mwaka mmoja wa elimu mtu anaopata unaongeza ufanisi katika utendaji kazi ambao hutoa mchango katika ukuaji uchumi na kuongeza maslahi ya anayepata elimu hiyo. Kwa kifupi ni kwamba rasilimali watu ni mtaji mkubwa mno katika ukuaji wa uchumi. Kwa nchi yenye watu wachache wenye elimu ya chuo kikuu kama Tanzania, kufukuza madaktari 200 waliosoma kwa wastani wa miaka 19 kila mmoja ni hasara kweli. Ngoja niweke tarakimu rahisi kabisa. Chukua miaka 7 ya shule ya msingi, halafu ongeza 6 ya sekondari, kisha ongeza mitano ya shahada ya kwanza ya udaktari na mwisho ongeza mwaka 1 wa mafunzo ya vitendo (Internship) inakupa jumla 19 kwa kila mmoja. Sasa ukizidisha miaka 19 kwa watu 200 unapata miaka 3,800 (Elfu tatu na mianane). Kwa hivyo miaka yote hii imepotea. Wakiamua kwenda kufanya kazi nchi nyingine, nchi hizo zitafaidi sana hiyo miaka 3,800 ya elimu. Kwamba walikuwa na haki ya kugoma au la ni mjadala mwingine. Leo nimejadili idadi ya miaka ya elimu itakayopotea kwa kufukuza madaktari 200.

Vyama Viendeshwe na wanachama

January 19, 2006
Ule uchaguzi wa mwaka jana umetoa funzo gani kwa vyama vinavyoitwa vya upinzani?( Sipendi hili neno upinzani; tuviiteje? Shindani?). Kwanza kabisa ingebidi wajifunze kwamba ruzuku haiwasaidii bali inawamaliza. Unajua ruzuku ndio inayofanya kila chama kitake kuweka mgombe wake ili angalau kipate mbunge na hatimaye ruzuku? Sisemi kwamba kuna vyama ambavyo vinaweka wagombea kwa sababu nyingine nje ya ruzuku. Ukiangalia kiundani kabisa ruzuku haifaidishi upinzani bali chama twawala. Katika ruzuku ya shilingi bilioni nane kwa mwaka CCM itaondoka na zaidi ya bilioni saba halafu kitakachobaki jamaa watagawana. Turudi kwenye hali halisi; ukitoa CCM ni chama gani kingine kinaweza kujigamba kwamba ruzuku inasaidia katika kampeni au katika kuimarisha chama? Ni asilimia ngapi kwa mfano ya fedha za kukodi helkopta ya CHADEMA ilitokana na ruzuku?

Ukweli ni kwamba kwanza kabisa chama ni kikundi cha watu wenye mwelekeo unaofanana au wanakubaliana kiitikadi. Kama ni kikundi basi inabidi kiendeshwe na hao wanachama. Hakuna haja ya kila mtanzania kuendelea kuendesha vyama ambavyo ni vya watanzania wachache sana. Hivi ni asilimia ngapi ya watanzania ni wanachama wa vyama vya siasa? Hili tulivalie njuga ili hii ruzuku ifutwe. Sioni kama eti ruzuku inasaidia kukuza vyama na hatimaye demokrasia. Kwanza hili suala la kufikiria demokrasia ni vyama vingi sijuhi limetoka wapi. Hata kama pesa hizi kinadharia zina lengo la kuimarisha vyama basi kinachoimarika ni kimoja tuu. Hata kama vingeimarika vyote, viimarishwe na wanachama wenyewe. Wanaopenda vyama wavichangie.

Hivi vyama vya upinzani ingebidi vianze kuchimba masuala ya msingi ambayo yanafanya CCM kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Kwa mfano mali ambazo CCM ilirithi wakati mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Angalia viwanja vya mpira kibao bado ni vya CCM, majengo mengi ambayo yalijengwa kwa kodi za wananchi bado ni ya CCM. Kwa nini mali hizo ziendelee kubaki za CCM? Tume ya Nyalali ilipendekeza kwamba mali hizo zirudishwe Serikalini lakini mpaka leo hakuna kilichorudishwa. Halafu jamaa wa upinzani wanakaa kukimbilia ruzuku ambayo kila mwaka itaendelea kuongezeka kw CCM huku ikipungua kwao, huku Chama hiki twawala kikiendelea kufaidika na mapato ambayo ni mali ya kila mtanzania. Pamoja na mambo mengine ya katiba na tume huru ya uchaguzi mimi nimeongele mambo mawili yanayohusu pesa.

Hili la ruzuku wanablogu wote tulivalie njuga. Vyama viendeshwe na wanachama hizo hela za ruzuku zikabiliane na kipindupindu au shughuli nyingine za kimaendeleo.