Natamani Kipindupindu kifike Ikulu

January 19, 2006
Kuna mwanamuziki mmoja mtanzania, kati ya wale wanaoitwa wa kizazi kipya anatamani mambo ya kuchekesha sana katika moja ya nyimbo zake. Kwa mfano anatamani mlima Kilimanjaro uamie sijuhi wapi na bahari pia ihame. Mimi leo nakuwa kama yeye. Natamani Kipindupindu kilipuke Mikocheni, Osterbay, Masaki halafu kipige hodi Ikulu pia. Kila siku kinavamia Buguruni, Manzese na sehemu zingine za walalahoi. Hivi kweli tumeshindwa kabisa kudhibiti kipindupindu? Labda kikifika ikulu kitapatiwa ufumbuzi. Rais mpya kaanza kazi kwa kukaribishwa na mlipuko wa kipindupindu kama ilivyo kawaida ya kila mwaka. Sijuhi kama atakivalia njuga kwa Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu mpya au kitaendelea kumaliza watu kwa Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya? Kama waziri wa Afya ataendeleza mapambano ya magonjwa kwa warsha, semina na makongamano na kuchapisha fulana na kofia basi hakuna kitakachotokea. Safari hii Waziri wa Afya ni Profesa. Sijuhi kama atasadia lolote kwa sababu huko nyuma alishawahi kuwepo Profesa akaboronga pia. Mimi sijuhi aibu hii ya kipindupindu itaisha lini.

Nawajibika kuomba Radhi

January 19, 2006
Kwa kweli nimepotea bila kutoa maelezo kwanza. Naomba radhi kwa hilo Ndesanjo kataka kuunda tume pamoja na kutaka kuwasiliana na FBI nitafutwe. Nimerudi. Naanza na nukuu hii ya Frantz Fanon. Kwamba wananchi ndio nguvu ya kubadili mambo. Niliwahi kuizungumzia bila kuiweka nukuu yenyewe: “To educate the masses politically does not mean, cannot mean making a political speech. What it means is to try, relentlessly and passionately, to teach the masses that everything depends on them; that if we stagnate, it is their responsibility and that if we go forward it is due to them too, that there is no famous man or woman who will take responsibility for everything and the magic hands are finally only the hands of the people”. Frantz Fanon
Nimeiweka ili kusisitiza kwamba tuna wajibu wa kuelimisha na kwamba sisi pia ni wananchi ambao tunaweza kuleta mabadiliko.

Kimya wenzangu!

January 3, 2006
Jamani nimekuwa kimya kwa muda sasa. Nilikuwa nakusanya nguvu baada ya igizo la tarehe 14. Wale waliotarajia mabadiliko makubwa nadhani wamekata tamaa. Wengine wanasema bunge limerudia kuwa la chama kimoja. Lakini Frantz Fanon anasema tuendelee kuelimisha wananchi mpaka wajue wao ndio wenye nguvu ya kuleta mabadiliko na hakuna mtu yeyote mmoja anayeweza kuleta mabadiliko ya maana isipokuwa wao wenyewe. Kwa wale wanaokubaliana na kalenda Gregory basi kheri ya mwaka mpya.

Igizo limeisha, tungoje miaka mingine mitano

December 17, 2005

Mchezo wa kuigiza umekwisha. Miaka mingine mitano wananchi watalishwa tena maneno, pilau, khanga, sukari watauza tena kura zao. Mchezo unaendelea. Lakini mchezo huu utaendelea hadi lini? Na watanzania tulivyo hatutawauliza wale walioshinda chochote hata kama hawatatimiza moja kati ya walioahidi. Lakini hata hivyo ni wangapi tunakumbuka hata ahadi zenyewe? Pilau na khanga na fulana zinatosha. Jamaa mmoja kaniacha hoi sana. Ameniambia jinsi ambavyo bado kuna kibarua kigumu mbele yetu. Alishuhudia watu wakibishana baada ya kampeni. Hawakubishana chochote kuhusu yaliyozungumzwa kwenye mkutano wa kampeni. Ubishi ulikuwa juu ya vifaa na magari ya vyama vyao. Mmoja akiwa anasema umeona spika za chama chetu? Ni nzito bwana si mchezo. Mwingine akamwambia acha utani, uliona gari walilokuwa wakitumia wagombea wa chama changu walipokuja hapa? Kazi ipo. Kwa kweli kama tunataka mabadiliko inabidi tusilale usingizi. Tupambane kweli.

Bendera ya Uingereza yafanyani katika tovuti ya CHADEMA?

November 23, 2005
Ndesanjo amekuwa akipigia kelele matumizi ya lugha ya kiingereza katika tovuti za kitanzania. Sasa leo katika kuipitia tovuti ya CHADEMA nimeona wameweka bendera ya Uingereza juu kabisa kwenye tovuti yao. Hiyo bendera inafanya nini hapo? Mimi sijuhi sababu labda kama kuna anayefahamu anisaidie.

UKIMWI bado ni tishio

November 22, 2005
Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia UKIMWI, UNAIDS kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani, WHO limetoa taarifa ya mwaka inayoonyesha jinsi UKIMWI ulivyo bado ni tishio hasa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Unaweza kuisoma taarifa hiyo kwa kubonyeza hapa

Kiswahili kitolewe utumwani kwanza

November 18, 2005
Jeff Msangi kaanzisha mjadala wa kiswahili katika blogu yake. Ametoa hoja za msingi ambazo zaweza kujadiliwa. Ili mjadala ule unoge naongezea makala iliyoandikwa na Prudence Karugendo anayetoa hoja kwamba tuanze kukitoa kiswahili utumwani kwanza. Hoja yake ni kwamba kiswahili kimeazima maneno mengi sana ya kiarabu wakati tuna lugha kwa mamia za kibantu ambazo tungeweza kutumia maneno yake na kubadilisha mengi ya kiarabu. Soma makala yake hapa na mjadala uendelee.

Uvutaji na unywaji wa pombe na Saratani tena

November 18, 2005
Engidio amesema kwamba kuna watu wametishwa sana na habari niliyoiweka hapa kuhusu unywaji pombe na Saratani. Sasa naweka kiungo kingine kuonyesha msisitizo wa jambo hili tena. Soma Hapa uone mambo zaidi kuhusu pombe sigara na saratani.

Saratani yazidi kuongezeka shauri ya kubwia pombe

November 16, 2005
Soma habari hii inayotoa onyo juu ya ongezeko la saratani kutokana na kunywa kupindukia. Bonyeza hapa

Uhuru si urithi

November 15, 2005

Nimekutana na nukuu hii:

“No people are really free until they become the instrument of their own liberation. Freedom is not a legacy that is bequeathed from one generation to another. Each generation must take and maintain its freedom with its own hands.” By John Henrik Clarke

Kila kizazi inabidi kipambane kujipatia uhuru wake.


Follow

Get every new post delivered to your Inbox.